Monday, August 28, 2017

Mawaziri wa fedha wa nchi 18 kukutana zanzibar septemba 8

Test
Mawaziri wa fedha wa nchi 18 kukutana Zanzibar Sept 8
28 Aug 2017, 06:40 pm| By Jennifer Sumi BIASHARA
Baraza la Mawaziri kutoka Umoja wa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika linaloshughulikia Udhibiti Utakasishaji Fedha Haramu, litakutana nchini Tanzania Septemba 08, 2017 katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, Visiwani Zanzibar.
Aidha, mkutano huo utatanguliwa na mkutano wa maafisa waandamizi (makatibu wakuu) utakaofanyika kuanzia Septemba 02 - 06 katika ukumbi wa Hoteli hiyo ya Zanzibar Beach Resort.
Kwa sasa Tanzania ndiuo Mwenyekiti  wa Umoja huo kwa kipindi cha mwaka mmoja, baada ya kupokea Uenyekiti kutoka Jamhuri ya Zimbabwe iliyomaliza muda wake mwezi Agosti, mwaka huu ambapo Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. PHILIP ISDOR MPANGO (MB),ndiye mwenyekiti  “President of the Council” atakayeongoza mkutano huo.
Katika mkutano huo pamoja na masuala mbalimbali yatakayojadiliwa, Serikali ya Tanzania, itatumia fursa hiyo  kuwasilisha taarifa ya hatua iliyofikia katika utekelezaji wa mpango wa “Financial Action Task Force” (FATF) ulioasisiwa mwaka 2009.
Mpango huo ulizitaka nchi wanachama kufanya  tathmini ya utekelezaji wa maazimio yaliyoainishwa kwenye FATF, katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya kisheria, kisera, miongozo ya kitaasisi zinazohusisha sekta za fedha na maeneo ya ushirikiano wa kimataifa.
Lengo ni kubaini jinsi nchi wanachama  zilivyojipanga katika kudhibiti suala la utakasishaji fedha haramu na ufadhili wa ugaidi (Anti-money Laundering and Combating the Financing of Terrorism).
Katika mkutano huo, mbinu na mikakati mbalimbali itakayosaidia kudhibiti matatizo hayo zitajadiliwa sanjari na hatua ambayo italeta matokeo chanya na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kufikia maendeleo tarajiwa katika nchi zote wanachama.
Tanzania ni miongoni mwa nchi waanzilishi wa umoja huo ulioasisiwa jijini Arusha,  mwaka 1999, pamoja na  nchi za  Uganda, Kenya, Mauritius, Namibia, Sychelles na Swaziland ambazo zilisaini makubaliano (Memorandum of Understanding - MOU) hayo.
Hatua ambayo ilipelekea Dar es Salaam kutajwa kuwa  makao makuu ya Sekretariati ya Umoja huo wenye nchi wanachama (18) ambazo ni Angola, Botswana, Ethiopia, Kenya, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Afrika Kusini, Swaziland, Sychelles, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe.

No comments:

Post a Comment

Uvinza FM