'Muungano ni kwa kurahisisha huduma za Bara na visiwani'
23 Oct 2017, 11:05
Kuwepo kwa Taasisi za Muungano Visiwani Zanzibar kunadaiwa kuwa ni suluhisho la kuwezesha na kubainisha kwamba muungano upo na uliwekwa kwa misingi wa kurahisisha shughuli za wananchi wanaohitaji huduma katika taasisi hizo kwa pande zote mbili.
Serikali ya Muungano imeendelea kuimarisha taasisi zake hizo na kuhakikisha zinakuwa msadaa na kiunganishi wa wananchi wa Bara na visiwani katika upatikanaji wa huduma bora zinazotolewa na taasisi hizo.
Miongoni mwa taasisi hizo ni pamoja na Uhamiaji, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Kampuni ya simu (TTCL) ambazo kwa kiasi kikubwa zinatoa fursa za ajira kwa wananchi wa pande zote mbili za muungano.
Katika mahojiano maalumu juu ya tathmini ya ziara yake kisiwani Unguja, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba amesema ziara hiyo imemsaidia kuona taswira mpya na kuahidi kuzifuatilia changamoto alizokutana nazo katika maeneo yote aliyotembelea.
Aidha waziri Makamba amewataka wananchi kuwa na imani na serikali zote mbili ili kufikia maendeleo yaliyokusudiwa.
Baada ya kumaliza ziara yake kisiwani Unguja, Waziri Makamba anatarajiwa kuendelea na ziara hiyo kisiwani Pemba.
No comments:
Post a Comment