SPORTPESA YAELEZA NIA YA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUUKARABATI UWANJA WA TAIFA KWA AJILI YA FAINALI ZA AFCON 2019
Kampuni ya michezo ya kubashiri nchini ya SportPesa Limited Ijumaa Septemba 13, 2017 imefanya mkutano na waandishi wa Habari kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuhusiana na zoezi linaloendelea la ukarabati wa Uwanja wa Taifa uliopo Temeke, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugezi wa Utekelezaji na Utawala wa SportPesa Tanzania, Bwana Tarimba Abbas amesema; “Tunashirikiana na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha uwanja huu unakamilika kwani tumetafuta wataalamu ambao wamebobea katika fani hii kuhakikisha uwanja wetu unakuwa katika ubora wa kimataifa.
Kuelekea kwenye fainali za AFCON za vijana mwaka 2019 ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji kwa mara ya kwanza, uwanja wa Taifa ambao ni miongoni mwa viwanja vikubwa na bora barani Afrika, utakuwa katika hali nzuri ikiwa ni sehemu ya maandalizi muhimu kuelekea kwenye fainali hizo.
Sisi kama SportPesa lengo letu kuu ni kuendeleza sekta ya michezo nchini Tanzania tukianzia na Mpira wa Miguu na kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo tunaamini tutafanikiwa kwa asilimia zaidi ya mia moja.
Naye Mkurugenzi wa Michezo wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bwana Yusuph Singo ameongeza kuwa; Tunawashukuru na tunawapongeza sana kwani kuendesha michezo sio lelemama. Kuendesha michezo ni jambo kubwa na linahitaji uwekezaji mkubwa na inahitaji pesa nyingi. Kwahiyo tunapopata wenzetu wakatusaidia, kwanza sisi kama serikali ni kuwashukuru na pia ni kufanya nao kazi kwa karibu sana.
SportPesa kwa kweli wameonesha mfano, wamejitahidi sana kudhamini vilabu mbalimbali, wametusaidia kurekebisha uwanja na kama sikosei gharama za kurekebisha uwanja zimefika takribani bilioni 1.3, ni hela nyingi sana hivyo sisi tunawashukuru na tunaendelea kuwaomba wasikate tamaa.
Kampuni ya SportPesa ambayo inajihusisha na michezo ya kubashiri nchini ndiyo mdhamini mkuu wa vilabu vya Simba, Yanga na Singida United huku ikiwa imejidhatiti katika kuhakikisha sekta ya michezo nchini inapata hadhi yake inayostahili.
No comments:
Post a Comment